Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Ataka TFDA na TBS Ziunganishwe
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirikia la Viwango Tanzania (TBS) kuacha urasimu huku akimtaka Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda kuandaa muswada wa kuunganisha taasisi hizo na kuwasilisha bungeni ili sheria zake zifanyiwe mapitio upya.
Majaliwa aliyasema hayo juzi katika kikao chake na wafanyabiashara wa kati na wadogo uliofanyika kwenye ukumbi wa Anatoglo ambapo alionyesha kukasirishwa na urasimu wa taasisi hizo mbili na kuagiza pia wakurugenzi wa taasisi hizo kufanya mapitio ya utendaji wa watumishi wao. Alisema mamlaka hizo zikiunganishwa zitaweza kuondoa malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakilalamikia kuwepo kwa tozo nyingi na urasimu unaosababisha taifa kupoteza makundi makubwa ya wafanyabiashara na wateja.
“Sheria za TBS na TFDA zote zinafanana, ni maneno tu mnacheza nayo huku ubora, sijui viwango, vikiwa na viwango lazima vitakuwa bora, urasimu tu ndio uliokithiri TBS na TFDA, mizigo inakuja bandarini inakaa miezi miwili mitatu mnajifanya mnapima, mnapima nini?”alihoji Majaliwa. Aliongeza kuwa ukimwi wenyewe siku hizi unapimwa kwa dakika tano unapewa majibu yako na kuongeza kuwa typhoid unapima leo, kesho mtu anatakiwa kupewa majibu lakini akahoji kwa nini wao wanachukua siku 20.
“Kama mashine zenu mbovu kwa nini msiagize mashine nyingine nje, Mkemia mkuu yupo kwa nini msiende kupima huko, mnakaa na bidhaa za watu muda mrefu mpaka zinaoza ndio maana wakati mwingine TRA wanaruhusu mizigo itoke mnakuja baadae kusema bidhaa haina viwango… mawaziri wa wizara zote kaeni na taasisi zenu mbadilike, kama mashine yenu inachukua miaka mitano kutoa majibu basi nunueni zenye ubora, nimesikia TBS wanapima mpaka stuli za kukalia, hivi stuli unapima nini? “alihoji.
Waziri Majaliwa alizitaka taasisi hizo zitoe mwongozo kama kwenye soko bidhaa za thamani za ndani zinazotakiwa sio kusumbua wafanyabiashara. “TBS mnapima mpaka shati, nadhani kuna haja ya kufanya mapitio taasisi hii, kuna mtu mmoja alikuja ofisini kwangu kanunua vifaa vyake China vya ujenzi vya nyumbani madirisha, milango na masinki ya vyoo, kalipia kila kitu vimefika bandarini TBS imezuia miezi minne eti mwisho mnasema vipo chini ya kiwango, kila kitu kikitoka Italia wananchi wa Magomeni Mapipa watawaweza kumudu gharama?” aliuliza.
Majaliwa pia aliwataka wafanyabiashara wasikubali kutoa rushwa kwa chombo chochote na kuwataka watendaji kuacha lugha za dharau kwa wananchi na kuzitaka taasisi zote zinazohusika na masuala ya Bandari, TRA, TBS na TFDA kukaa jengo moja kuwaepusha wananchi na usumbufu wa nenda rudi.
“Bandarini kuna jengo moja kubwa sana pale limekaa kama meli, kuna vyumba vipo tupu, taasisi zote zinazousika zikae pale mtu akienda kulipia mizigo yake anamaliza kila kitu pale sio kupiga makitaimu mara bandarini, Ubungo achene urasimu, na nyie wananchi, rushwa si sehemu ya mkakati wa serikali, hivyo vita dhidi ya rushwa lazima iendelezwe na watu wote. Mafanikio tuliyoyapata ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa huduma za afya, maji na barabara ni matokeo ya kupiga vita rushwa,” alisema.
Majaliwa aliwataka pia watumishi kuacha kukaa ofisini na badala yake wajenge tabia ya tabia ya kuwatembelea wafanyabiashara kwenye maeneo yao na kusikiliza kero zinazowakabili na kushirikiana nao ili kutafuta ufumbuzi.
“Kila mtendaji katika eneo lake atekeleze majukumu yake kikamilifu urasimu, dharau, lugha za ajabu zimeshamiri kwenye maeneo ya kutolea huduma jambo ambalo si sahihi. Badilikeni,” alisema. Alisema serikali imepanga mpango wa kulibadilisha utaratibu wa kufanya biashara katika eneo la Kariakoo ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa saa 24 kama yalivyo masoko makubwa duniani.
Waziri Mkuu alisema lengo la mabadiliko hayo ni kukuza uchumi wa taifa na wa wafanyabiashara kwa ujumla. “Nchi yetu ina usalama na ulinzi wa kutosha hivyo hatuwezi kushindwa kufanya biasahara wakati wote.”
Katika mkutano huo aliouitisha kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao, Waziri Mkuu alisema atakutana na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam ili kupanga namna ya kutekeleza utaratibu huo. Alisema jiji la Dar es Salaam moyo wa kitivo cha kibiashara nchini, hivyo serikali itahakikisha mwenendo wa biashara unaboreshwa pamoja na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kufanya biashara zao wakati wote na bila usumbufu.
Post a Comment